UTAFITI: WANAWAKE WA RWANDA NA KENYA KUISHI MIAKA MINGI

Related image

Wanawake nchini Rwanda na Kenya ndio wanaotarajiwa kuishi muda mrefu zaidi miongoni mwa wanawake na wanaume katika nchi za Afrika Mashariki, kwa mujibu wa takwimu. Umri wa wanawake kuishi Rwanda kwa sasa ni miaka 69.3 na nchini Kenya ni miaka 69.0.

Hata hivyo, umri wa kuishi wa wanaume Uganda ndio ulioongezeka zaidi katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, ambapo umepanda kwa miaka 13.5.

Nchini Tanzania, umri wa kawaida wa kuishi kwa wanawake kufikia mwaka 2016 ulikuwa miaka 66, ongezeko la miaka 10 ukilinganisha na mwaka 1990 kwa mujibu wa Utafiti wa Mzigo wa Maradhi Duniani mwaka 2016, ulioratibiwa na Taasisi ya Takwimu za Afya na Utathmini.

Kwa wanaume, umri wa kuishi ulikuwa miaka 62.6 kufikia mwaka 2016 ukilinganisha na miaka 53.7 mwaka 1990. Kwa kiwango cha kadiri, umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kwa miaka kumi kufikia sasa tangu mwaka 1990.

Nchini Kenya, umri wa kuishi kwa wanawake umeongezeka kutoka miaka 62.6 mwaka 1990 hadi miaka 69 mwaka 2016, ongezeko la takriban miaka sita, lakini kwa wanaume ongezeko limekuwa ni kutoka miaka 60.2 hadi miaka 64.7, miaka 4.5.

Nchini Uganda, umri wa kuishi kwa wanawake sasa ni miaka 64.7 (sawa na umri wa wanaume kuishi Kenya) na kwa wanaume ni miaka 59.8.

Kiwango hicho hata hivyo kimeimarika kwa zaidi ya miaka 10 kwa kila jinsia kwani mwaka 1990 umri wa wanawake kuishi Uganda ulikuwa miaka 52.1 na kwa wanaume 46.3.

Kwa sasa, kwa kawaida, kila mwanamke aliyefikisha umri wa kujaliwa mtoto nchini humo huwapata watoto 4.7 ukilinganisha na watoto 3.7 kwa kila mwanamke Mkenya.

Pato la jumla kwa kila raia Tanzania kufikia mwaka jana lilikuwa $2,516 lakini Kenya lilikuwa $2,925, tofauti ikiwa $409.

Uganda, ambapo pato kwa kila raia kila mwaka ni $1,838, kila mwanamke hujifungua watoto 5.6.

Kinachowaua Watanzania zaidi

Chanzo kikuu cha vifo Tanzania kimesalia kuwa Ukimwi/VVU sawa na ilivyokuwa mwaka 2005, ambapo ugonjwa huo unafuatwa na maambukizi kwenye mfumo wa kupumua mwilini.

Ugonjwa wa Malaria ulikuwa wa tatu kwa kusababisha vifo mwaka 2005 Tanzania lakini sasa nafasi hiyo imechukuliwa na magonjwa ya kuharisha na nafasi ya nne maradhi ya moyo, vyanzo ambavyo mwaka 2005 vilikuwa vinashikilia nafasi ya nne ya tano mtawalia. Ugonjwa wa Malaria unashikilia nafasi ya tano kwa kusababisha vifo nchini humo kufikia mwaka 2016.

Ugonjwa wa Kifua kikuu ulikuwa kufikia mwaka 2016 ulikuwa wa sita kwa kusababisha vifo Tanzania, ambapo umepanda kutoka nafasi ya saba mwaka 2017.

Maradhi ya ubongo pia yameongezeka kwa kusababisha vifo katika nafasi ya saba kutoka nafasi ya tisa mwaka 2005, lakini maradhi kichwa baada ya kuzaliwa kwa mtoto yamesalia nafasi ya nane.

Umri wa kuishi kwa wanawake na wanaume baadhi ya mataifa Afrika

Taifa Wanawake Wanaume
Afrika Kusini 65.5 59.2
Burundi 61.5 59.2
DR Congo 62.7 60.4
Kenya 69 64.7
Malawi 62.6 57.9
Misri 75 69.4
Nigeria 66.4 63.7
Rwanda 69.3 66
Somalia 57.7 56.6
Tanzania 66 62.6
Uganda 64.7 59.8

Utapia mlo kutokana na ukosefu wa protini na nguvu mwilini ulikuwa nafasi ya sita kwa kuchangia vifo Tanzania mwaka 2005 lakini sasa umo nafasi ya tisa, huku nafasi ya 10, sawa na ilivyokuwa mwaka 2005, ikishikiliwa na visa vya kuzaliwa kwa watoto njiti (watoto ambao hawajafikisha muda ufaao wa kuzaliwa).

Chanzo BBC

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...