BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU (HESLB) YAANZA KUPOKEA MAOMBI YA MIKOPO 2018/2019

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa muda wa miezi miwili na kusisitiza kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul Razaq Badru amesema leo jijini Dar es salaam wakatik akifungua rasmi kuwa mtandao wa kuwasilisha maombi ya mkopo (www.olas.heslb.go.tz) utakuwa wazi kuanzia Mei 10, 2018 hadi Julai 15, 2018 ili kuwapa fursa wanafunzi wahitaji kuwasilisha maombi yao.

“Mwaka jana tulitoa mwezi mmoja, mwaka huu tumetoa muda zaidi ili kuwawezesha kusoma mwongozo kwa makini na kuzingatia maelekezo tunayoyatoa,” amesema Badru katika mkutano na wanahabari ambapo pia alizungumzia mambo muhimu yaliyomo kwenye mwongozo unaojumuisha sifa na taratibu za utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019. Mwongozo huo unapatikana katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kwenye tovuti ya Bodi.

Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa katika utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019, kipaumbele kitatolewa kwa watanzania wahitaji wanaosoma kozi zenye uhitaji mkubwa zaidi kitaifa kama walimu wa masomo ya sayansi na hisabati; na sayansi ya afya ya binadamu.

“Tutatoa kipaumbele pia kwa waombaji mikopo watakaodahiliwa katika kozi zinazohitajika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi wa aina zote; kozi za sayansi za kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi na nishati,” amesema Badru katika mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa wadau wa HESLB kama Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO); Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Shirika la Posta (TPC).

Aidha, ameongeza kuwa watanzania wahitaji ambao ni yatima na wana nakala za vyeti vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) nao watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma.

Wengine watakaopewa kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu uliothibitishwa na Mganga wa Mkoa au Wilaya na waombaji mikopo ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya stashahada (Diploma) au sekondari na wana barua za uthibitisho kutoka taasisi zilizowafadhili.

Kuhusu malengo ya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019, Badru amesema Bodi imepanga kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi wapya 40,000 na wanaoendelea zaidi ya 80,000.

Kati yao, wanawake watakuwa asilimia 35 (14,000) na wanaume asilimia 65 (26,000). Bajeti ya fedha za mikopo kwa mwaka 2018/2019 ni TZs 427 bilioni.

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...