TMA YATOA TAHADHARI YA MVUA KUBWA ZAIDI INAYOKUJA

Kama ulidhani kwamba hekaheka zinazotokana na mvua inazoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi hususan mikoa ya Pwani inakaribia kumalizika, utakuwa unajidanganya.

Chukua tahadhari, tena kubwa kwani Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua hiyo haitegemewi kupungua katika siku za karibuni na angalizo kubwa zaidi ni kwamba kuna uwezekano kuongezeka maradufu ifikapo Mei 10 na kwamba inatarajiwa kuendelea kunyesha hadi mwishoni mwa mwezi huu.

“Zitaendelea kunyesha katika viwango tofauti kutokana na mambo mengi ikiwamo mabadiliko katika bahari na ndiyo maana kuna wakati unaweza ukaona kijua kidogo kisha mvua zinaendelea. Wananchi lazima wachukue tahadhari,” Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema jana alipokuwa akizungumzia hali ya mvua zinazonyesha.

Alisema wananchi wengi wanaopata madhara ni wale ambao wamekuwa wakipuuza miongozo inayotolewa na mamlaka hiyo kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua hivyo kujikuta wakikumbwa na maafa ikiwamo kupoteza ndugu na mali.

Mwezi uliopita, mvua kubwa iliyonyesha mfululizo jijini hapa ilisababisha vifo vya watu tisa huku nyumba zaidi 300 zikisombwa na maji.

“Hizi mvua zinazoendelea kunyesha zipo katika msimu wa mvua ambao tahadhari zake tulitoa mapema kabla ya hata hazijaanza kunyesha sasa wananchi wakati mwingine hawazingatii maana wakiona leo inanyesha na siku ya pili kuna jua, basi wanarudi tena kwenye nyumba zao na kuendelea na maisha,” alisema.

Juzi, kampuni ya mabasi yaendayo haraka (Udart) ilisitisha baadhi ya huduma zake kuanzia saa sita mchana kabla ya kuzirejesha baada ya hali kutulia kutokana na maji kujaa eneo la Jangwani.

Mbali ya eneo hilo, barabara kadhaa zikiwamo za Mandela, Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujuma zilikuwa na msongamano wa magari kutokana na mvua hizo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema hakuna athari yoyote iliyosababishwa na mvua hizo zilizonyesha jana na juzi.

Kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini, Bwawa la Nyumba ya Mungu, linalotumika kuzalisha umeme na shughuli za uvuvi, linatarajiwa kujaa maji leo na kutapika, tukio ambalo hutokea kila baada ya kipindi cha miaka 10.

Vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa tukio hilo litasababisha pia samaki hasa kambale, kusombwa na maji na kuelekea Mto Pangani kutokana na shughuli za uvuvi kusitishwa katika bwawa hilo.

Uchunguzi wa wataalamu wa Bonde la Pangani (PBWO) uliofanywa juzi ulionyesha kuwa usawa wa bwawa hilo ulikuwa umefikia mita 688.60, likiwa limebakiza sentimita 31 tu kujaa na wingi huo wa maji unaweza kufikia wa mwaka 1998 wakati wa mvua za El Nino.

Takwimu zinaonyesha bwawa hilo lilijaa maji na kutapika mwaka 1988 na baadaye 1998 na kisha hali hiyo kujirudia mwaka 2008, na sasa wataalamu wanajiandaa kuthibitisha kujirudia mwaka huu.

Kaimu Ofisa wa Maji PBWO, Vendelin Basso, alisema wanafuatilia jinsi kina cha bwawa hilo juu ya usawa wa bahari kinavyopanda pamoja na wingi wa maji yanayoingia kwa kasi.

“Linatarajiwa kuwa limejaa na kupitisha maji kupitia njia maalumu ya dharura yaani spillway, ambayo itayaingiza katika Mto Pangani litakapofikia usawa wa mita 688.91,” alisema.

Basso alisema kiasi cha maji kinachoingia bwawani ni wastani wa mita za ujazo 150 hadi 200 kwa sekunde kwa muda wa wiki mbili zilizopita hivyo, linatarajiwa kujaa kati ya leo na kesho.

“Hatutarajii athari kubwa kwa kuwa maji yatafuata mkondo wa Mto Pangani, isipokuwa ni lazima wananchi wachukue tahadhari kwa kuwa maji hayo yatakuwa mengi mtoni,” alisema

Alisema taarifa hizo zimetolewa maeneo ambayo yapo kando ya Mto Pangani ya kata za Ngorika, Ngage, Kirya na Loiborsoit kwa Wilaya ya Simanjiro pia, katika kata za Ruvu na Mabilioni zilizopo Wilaya ya Same na Mkomazi iliyopo Korogwe.

Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe alisema anatarajia kwenda kushuhudia tukio la kujaa kwa bwawa hilo leo akiwa na wataalamu mbalimbali wa wilaya hiyo.

Profesa Maghembe alisema bahati mbaya zuio la uvuvi katika bwawa hilo limeangukia katika tukio hilo la maji kujaa linalotokea kila baada ya miaka 10 na kuleta kambale wengi.

“Hiki ndicho kilipaswa kiwe kipindi cha kupiga bingo kwa wavuvi lakini ndio kipindi wamezuiwa. Kitaalamu na kiikolojia wasingestahili wazuiwe kwa sababu ikifika Juni samaki hawapatikani,” alisema.

Bwawa la Nyumba ya Mungu lilijengwa mwaka 1966 kwa ajili ya shughuli za kuzalisha umeme, uvuvi na kilimo cha umwagiliaji na linategemewa na zaidi ya watu 20,000.

Na Mwananchi

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...